Hongera ndugu Matiang’i kwa kusafisha uvundo katika wizara ya elimu

Daktari Matiang'i [Picha: Hisani]

Awali ya yote msomaji wangu mpendwa pokea mkono wa mwaka wa kheri 2017.

Vivyo hivyo, pokea dua na maombi yangu, jumuisha na yako, kuuaga mwaka 2016. Mbona nimeanza hivi simulizi zangu leo hii?

Ni kwa kuwa sasa hivi wengi wanaulaki mwaka 2017 na kuweka maazimio kama ilivyo ada na desturi. Kama tutayatamiza maazimio hayo litakuwa gumzo la siku nyingine Mola akipenda.

Wepo watu wengi tu nchini waliofanya mambo mazuri mwaka wa 2016. Miongoni mwao ni wanamichezo wetu waliokuwa huko Rio Brazil kushiriki mashindano ya Plimpiki.

Mbali na medali walizozinyakua kwa faida ya nchi hii, sisi hapa leo hii twawavisha pete chandani. Wakumbuka timu yetu ya soka kinadada? Kwa mara ya kwanza kushiriki katika fainali za Afrika huko Cameroon.Hongera dada zetu. Twawazimia sigareti!

Malimwengu ya siasa yalikuwa na sema sema nyingi za hapa na pale. Hata hivyo, mama waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Amina Mohammed Jibril anastahili kuvuliwa kofia.

Sasa hivi jina la waziri wa Elimu Dr. Fred Okengo Matiang’i linarindima. Jina la Matiang’i limesemwa sana mwaka huu. Na litasemwa sana mwakani. Kwa nini?

Waziri Matiang’i ameleta kumbukizi za utenda kazi wa mwendazake aliyekuwa waziri katika wizara mbalimbali, lakini alisafisha pakubwa wizara ya uchukuzi marehemu John Njoroge Michuki.

Sasa hivi akafufuka ndugu Michuki na kuikuta hali ilivyo katika wizara ya uchukuzi, atatamani sana ardhi kummeza mzima mzima!

Alichokifanya mwaka huu ndugu Matiang’i katika wizara ya elimu, kwa ushirikiano na Baraza la Taifa la Mitihani, linahitaji bonasi. Ndugu George Magoha pia nawe pokea mkono wa hongera. Japo wepo wanaodhani kuwa Matiang’i hastahili pongezi kwa kuwa alikuwa akifanya tu kazi yake.

La hasha! Nchini mna uozo ulioozeana na kuvunda uvundo wa fondogoo, hivi kwamba anahitajika mtu jasiri aso na umero wa ufisadi ili kunyoosha jambo alivyonyoosha Matiang’i.

Ushauri wangu kwako ndugu Matiang’i ni kuwa ukumbuke kuwa mgema akisifiwa tembo hulitia maji.

Vivyo hivyo, wengi wa wakosoaji na wahakiki wako watakuwa wakikutega kwa kila aina ya mitego. Binadamu ni ngamba ati!

Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (RADIO MAISHA).
[email protected], [email protected],
FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali,
Twitter: @alikauleni

 


JOIN THE CONVERSATION


next